Mahakama nchini Sudan imemuhukumu kifo mwanamke mmoja anayedaiwa kubadili dini yake na kuolewa na mwanaume mkristo. Daktari Mariam Yahya Ibrahim Ishag ambae baba yake ni muisilamu alishitakiwa kwa kosa la kuasi dini pamoja na kufanya zinaa kwa kuolewa na mwanamume mkristo kitu ambacho dini ya kiisilamu imeharamisha kwa Wanawake.
BBC wamesema Mariam mwenye umri wa miaka 28 pia ni mjamzito na ataadhabiwa kwa kuchapwa mijeledi 100 kwa kosa la zinaa.
Unaambiwa Mariam alilelewa na mama
yake mzazi ambae ni Mkristo lakini maafisa wa Sudan wanasema yeye bado
ni Muislamu kwa sababu ndio dini ya baba.
Alipewa siku tatu baada ya kuhukumiwa
aweze kurejea katika dini ya kiisilamu lakini akakataa na ndio maana
adhabu ikabaki palepale kwa kuwa Wanawake Waislamu hawaruhusiwi kuolewa
na Wanaume Wakristo ingawa Wanaume Waisilamu wanaruhusiwa kuwaoa
wanawake wakristo.
Shirika la kimataifa la kutetea haki
za binadamu Amnesty International linasema kuwa Ishag alilelewa kama
Mkristo muorthodoxi kwa sababu baba yake hakuwepo naye maishani mwake.
Kesi ya Ibrahim ni ya kwanza ya aina
yake kusikika nchini Sudan kwa mujibu wa shirika la habari la Reuters na
Wanaharakati wa kutetea haki za binadamu, wamelaani uamuzi huo wa
Mahakama na kuitaka serikali ya Sudan kuheshimu haki na uhuru wa watu
kuabudu.
Maafisa wa balozi za mataifa ya
magharibi pia wamekemea vikali kesi hiyo na kuelezea asiwasi wao na
kuwataka maafisa wa sheria nchini humo kuangalia kesi hiyo upya na
kuhakikisha kuwa Mariam anatendewa haki.
Waziri wa mawasiliano amesema kuwa sio
Sudan peke yake ambako sheria za kiisilamu zinafuatwa na ambako sio
sawa kwa mtu kubadili dini yake, hali hiyo pia ipo nchini Saudi Arabia
na katika nchi nyngine zinazofata sheria za kiisilamu.
Serikali ya Rais Omar al-Bashir
inakabiliwa na changamoto nyingi za kiuchumi na kisiasa hasa baada ya
kujitenga na Sudan Kusini ambako mafuta yake yalikuwa yanatoka mwaka
2011.