Kajala amcharukia Wema Sepetu......Asema hana mpango wa kumlipa zile milioni 13 alizotoa Wema Sepetu Mahakamani, aeleza mambo mazito




Zile shilingi milioni 13 alizolipa staa mkubwa wa kike Bongo, Wema Isaac Sepetu ‘Beautiful Onyinye’ mahakamani ili kumnusuru Kajala Masanja kwenda gerezani, zinaendelea kusababisha fukuto na sasa Kajala amejibu mapigo, akisema hatamlipa Wema fedha hizo.

Wema na Kajala wapo kwenye gogoro zito kwa muda mrefu huku mashabiki wa mastaa hao waliojipa majina ya Team Wema (wanaomuunga mkono Wema) na Team Kajala (walio upande wa Kajala) wakiukuza ugomvi huo kwa kushambuliana kwa maneno makali kwenye mitandao mbalimbali ya kijamii.
 
WEMA KUFUNGUKA
Katika gazeti, toleo namba 877 la Aprili 25-Mei Mosi, 2014 la wiki iliyopita, liliandika habari ya Wema iliyokuwa na kichwa; Kwa mara ya kwanza Wema afunguka, asema: NAJUTA KUMLIPIA KAJALA MIL. 13!
 
Hiyo ilikuwa mara ya kwanza kwa Wema kufunguka baada ya bifu la kimyakimya la muda mrefu ambapo alifafanua chanzo cha bifu lao na namna anavyojuta kumlipia Kajala fedha hizo.
 
“Kusema kweli najuta kumlipia (Kajala) ile faini ya Sh. milioni 13. Bora angeenda jela miaka saba kuliko kunisababishia matatizo na maumivu kiasi hiki. Mimi sijawahi kumsema vibaya K kisa eti nilimlipia fedha hizo,” alisema Wema katika gazeti hilo.
 
Alipoambiwa kama Kajala yupo tayari kurudisha fedha hizo alisema:
 
“Kama anataka kunilipa, anilipe kisha aende jela maana mimi sikumkopesha, nilitoa kwa moyo.”
 
HABARI ZA MOTO
Baada ya gazeti hilo kuruka mitaani na Kajala kulipata ndipo akaeleza mambo mazito.
 
Akizungumza na mwanahabari wetu, Kajala alisema katika vitu ambavyo Wema anatakiwa kuvisahau ni pamoja na kumlipia mahakamani hizo milioni 13.
 
“Siwezi kumlipa ng’o. Namlipa nini sasa na kivipi? Kwani tulikopeshana? Hakuna anachonidai Wema, hata kama akisema nimlipe, siwezi kufanya hivyo,” alisema Kajala.
 
Huku akimwaga machozi, Kajala aliendelea: “Unajua haya mambo yanachukuliwa kirahisi tu na wadandiaji wa mambo, ni vile watu hawajui ni kwa kiwango gani hili suala linaniumiza.
 
“Wema alinisaidia, alinilipia fedha mahakamani wakati ambao nilikuwa na uhitaji na sikuwa na zile fedha. Kama asingejitokeza kunilipia nilikuwa nakwenda jela.
 
“Lile ni jambo kubwa. Thamani yake haifananishiki na fedha. Ule ulikuwa ni utu tu, sasa leo iweje ligeuzwe kuwa kama deni? Siwezi kufanya hivyo.”
 
YUPO TAYARI KWA SULUHU
Kwa mara nyingine tena, Kajala alisema kuhusu kupatana na Wema yupo tayari muda wowote, maana haoni sababu ya kuendelea kwa ugomvi huo.
 
Hii ni mara ya tatu Kajala kuzungumzia suluhu akisisitiza: “Nakosa amani kabisa na huu mzigo. Natamani kuutua. Nipo tayari kukutanishwa naye hata leo tuyamalize.”
 
HABARI YA MJINI
Habari ambazo zimeenea mjini lakini bado hazijathibitishwa zinadai kuwa, Kajala anajiamini kwa sababu anajua fedha alizolipiwa na Wema si zake, zililipwa na aliyekuwa mwanaume (boyfriend) wa Wema, yule kigogo wa Ikulu anayetajwa kwa jina la CK.
 
“Lile lilikuwa agizo, Wema hakuwa na fedha zote zile kwa ajili ya kumlipia Kajala. Alipewa na CK na kuambiwa amlipie ili asiende jela,” alisema mmoja wa watu wa karibu na mastaa hao kwa sharti la kutotajwa gazetini.
 
ETI ULIKUWA MPANGO!
Chanzo kinaendelea: “Alivyoingia mitaani, CK akajiweka karibu na Kajala na kumweleza mchongo mzima, kuwa yeye ndiye aliyetoa  hizo fedha kwa hiyo asiwe na wasiwasi.
 
“Ndiyo maana hata Wema na CK walivyoachana ikawa rahisi kwa CK kujimilikisha Kajala moja kwa moja kwa sababu anaujua ukweli.”
 
Haya ni madai ya chanzo chetu ambayo hayajathibitishwa na wahusika.
 
SAFARI ZA CHINA VIPI?
Habari nyingine ambazo bado zinafuatiliwa ili zithibitishwe, zinasema kuwa, safari nyingi za Kajala kwenda China kwa mapumziko huwa anamfuata au kuongozana na CK.
 
“Hata sasa hivi (juzi Jumatano) wapo safarini China wanakula bata. Yaani haya mambo yamejifunga sana. Yanahitaji hekima sana kuyamaliza,” aliendelea kudai.
  
Source: Gazeti  la  Ijumaa/GPL