NA SAMSON CHACHA, Gazeti la Uhuru, TARIME
MKAZI wa Kijiji cha Nyamwaga wilayani hapa mkoani Mara, Mbusiro Muyuyi, ameuawa kwa kukatwakatwa kwa panga kichwani na shemeji yake.
Mauaji hayo
yaliyowashitua wengi wilayani hapa, chanzo chake ni mbwa wa mtuhumiwa,
Mwita Muyuyi (17), kula mayai ya kuku wa marehemu.
Habari za
kuaminika zimesema kuwa, Mbusiro (45), alimtuhumu shemeji yake kuwa,
mbwa wake amekula mayai ya kuku, hali iliyoibua mzozo mkubwa baina yao.
Kamanda wa
Polisi wa Kanda Maalumu ya Tarime/ Rorya, Justus Kamugisha, alisema
tukio hilo lilitokea juzi asubuhi katika kitongoji cha Ntarachagine.
Alisema wakati
mzozo huo ukiendelea, Muyuyi alikuwa ameshika panga na ghafla alianza
kumshambulia mke wa kaka yake sehemu mbalimbali za mwili wake.
Kamanda
Kamugisha alisema baada ya tukio hilo, Mbusiro alikimbizwa hospitali kwa
matibabu, lakini akiwa kwenye zahanati ya Nyarero, hali yake ilizidi
kuwa mbaya na kufariki dunia.
Tayari
mtuhumiwa anashikiliwa na polisi kwa uchunguzi zaidi kabla ya
kupandishwa kizimbani kujibu tuhuma za mauaji zinazomkabili.
Kamanda
Kamugisha alitumia fursa hiyo kuwataka wananchi kuacha tabia za
kujichukulia sheria mkononi na badala yake wafikishe migogoro kwenye
vyombo vya ulinzi na usalama kwa hatua zaidi.