Watanzania wameshauriwa kufuga na kula panya aina ya ndezi wakieleza kuwa nyama hiyo haina mafuta mengi, ikiwa pia na virutubisho muhimu na vilivyo adimu.
Rai hiyo imetolewa na wataalamu kutoka Chuo Kikuu
cha Kilimo cha Sokoine (SUA) katika Maonyesho ya Vyuo Vikuu nchini
yaliyofanyika jijini Dar es Salaam hivi karibuni.
Wataalamu hao walisema kuwa ili kukabiliana na uharibifu wa kuchoma moto misitu kwa ajili ya kuwatafuta wanyama hao, ni vyema wananchi wakaanza kuwafuga kwa kuwa nyama yao ina ladha nzuri na ni laini.
Wataalamu hao walisema kuwa ili kukabiliana na uharibifu wa kuchoma moto misitu kwa ajili ya kuwatafuta wanyama hao, ni vyema wananchi wakaanza kuwafuga kwa kuwa nyama yao ina ladha nzuri na ni laini.
Mhadhiri Mwandamizi wa SUA, Idara ya Uzalishaji,
Mirende Matiko alisema kuwa ingawa wanyama hao wanafugwa kwa wingi
katika nchi za Afrika Magharibi, hapa nchini ufugaji wake unakabiliwa na
changamoto nyingi.
“Wakulima wetu hapa tunawapa wafuge, siku chache
baadaye ukienda utaambiwa walikufa, lakini ukiwauliza majirani
wanakuwambia ‘jamaa aliwachinja’, ni sawa na kumpa mkulima mbegu halafu
anakula,” alisema Matiko.
Akizungumzia namna nyama hiyo inavyoliwa, Matiko
alisema: “Nyama yake ina viinilishe vingi, yanatupwa manyoya na miguu
yake tu, vitu vingine vyote vinaliwa. Tena utumbo ndiyo mtamu sana, si
unajua wanakula nyasi tu.”
Alisema wanyama hao wana faida nyingi kiuchumi
ikiwamo kuongeza pato la kaya, kuchangia uwindaji endelevu, kutunza
bioanuwai pia nyama yao ni gharama nafuu, ikilinganishwa na nyingine.
“Mtu akitaka kufuga wanyama hao anatakiwa kuwa na
banda madhubuti lenye ubora, chakula na maji safi yawepo bandani muda
wote na upandishaji ufanyike katika muda mwafaka,” alisema.
Mhadhiri huyo alitoa hadhari kwa wafugaji
akiwataka kuwakamata wanyama hao kwa umakini kutumia chandarua, kuepuka
kusababisha majeraha.
Ndezi ni jamii ya nungunungu na pimbi, wakiwa wa
aina mbili, ambapo wadogo huwa na uzito wa kati ya kilo nne hadi sita na
wakubwa hufikia hadi kilo tisa. Wanyama hao hupendelea kuishi kwenye
maeneo yanayolimwa mashamba ya miwa, ulezi na mpunga.
Hata hivyo, Dk Loth Mulungu alisema kuwa wawindaji
wa ndezi porini husababisha madhara makubwa ikiwamo uchomaji wa misitu,
uharibifu wa bioanuwai, kukanyaga mazao mashambani na upotevu wa muda.
Mmoja wa watazamaji waliotembelea Banda la SUA,
Elizabeth Maro alisema kuwa ingawa kwa muda mrefu amesikia watu wakila
mnyama huyo. Binafsi hawezi kula nyama yake kwa kuwa anaamini hana
tofauti na panya wengine.
“Siwezi kumla kwa namna yoyote, huyu ni panya tu
ndiyo maana hata jina lake kwa Kiingereza anaitwa ‘canerat’, maana yake
panya mla miwa,” alisema.
Ipyana Mwambungu alisema mnyama huyo ameadimika katika baadhi ya mikoa kutokana na watu wengi kuipenda nyama yake.
“Kuna baadhi ya maeneo kule Kilimanjaro huwezi kuwaona tena ndezi, wakati zamani walikuwa wengi sana,” alisema.
Credit: Mwananchi
Credit: Mwananchi