Mlevi afariki dunia baada ya kunywa VIROBA vingi bila kula chakula




Michael  Silanda ( 26 )   mkazi  wa  kijiji  cha  Ibindi, tarafa  ya  Nsimbo  wilaya  ya  Mlele  mkoani  Katavi  amefariki  dunia  baada  ya  kunywa  pombe ( Viroba )  aina  ya  Zed  kupita  kiasi  bila  kula  chakula....

Kamanda  wa  polisi  mkoani  Katavi,Kamishna  Msaidizi  Mwandamizi,Dhahiri Kidavashari  amesema  tukio  hilo  limetokea  wiki  iliyopita  majira  ya  saa  sita  usiku  kijijini  hapo.....

Alisema  siku  ya  tukio  marehemu  baada  ya  kuamka  asubuhi  nyumbani kwake  hapo  majira  ya  saa  tano  asubuhi  alielekea  kwenye  baa  ambayo  ilikuwa  ikiuza  vinywaji  vya  aina  mbalimbali  zikiwemo  pombe  kali....

Alifafanua  kuwa,baada  ya  kufika  kwenye  baa  hiyo  aliwakuta baadhi  ya  wanakijiji  wenzake  wakiwa  wanakunywa  pombe  za  aina  mbalimbali  hali  ambayo  ilimfanya  marehemu  aweze  kujumuika  nao  kwa  kuagiza  pombe  aina  ya  Zed...

Alisema  Michael  aliendelea  kunywa  viroba  kuanzia  muda  huo  kwenye  baa  hiyo  bila  kula  kitu  chochote  hadi  majira  ya  saa  sita  usiku  alipoamua  kurudi  nyumbani  kwake  huku  akiwa  amelewa  pombe  kupita  kiasi....

Baada  ya  kufika nyumbani  kwake  aliingia  ndani  ya  nyumba  yake  na  kulala  bila  kula  chakula  cha  aina  yoyote  na siku  iliyofuata  majira  ya  saa  mbili  asubuhi  ndipo  walipomkuta  Michael  akiwa  amefariki  huku  akiwa  amelala  kitandani  kwake,.....

Kamanda  Kidavashari  alisema  uchunguzi  wa  awali  uliofanywa  kuhusiana  na  tukio  hilo  umebaini  kuwa  kifo  hicho  kimesababishwa  na  marehemu  kunywa  pombe  nyingi  kupita  kiasi  bila  kula  chakula....