Taarifa ya Wizara ya Afya kuhusu ugonjwa wa homa ya Dengue......



TAARIFA KWA UMMA KUHUSU UGONJWA WA HOMA YA DENGUE “DENGUE FEVER”



Utangulizi

Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii inapenda kutoa taarifa kwa Umma juu ya mwenendo wa ugonjwa wa homa ya dengue yaani “dengue fever” hapa nchini.Ugonjwa huu umethibitishwa baada ya sampuli zilizochukuliwa kutoka kwa watu waliohisiwa kuwa na ugonjwa huu jijini Dar es Salaam kupelekwa kwenye maabara yetu ya Taifa Dar es salaam na kuthibitisha kuwa na virusi vya homa ya dengue mnamo mwishoni mwa mwezi wa Januari 2014. Hadi sasa idadi ya wagonjwa ambao wamethibishwa kuwa na ugonjwa huuni 400 na Vifo 3. Kwa wiki iliyoshia tarehe 9 Mei 2014 ya idadi ya wagonjwa waliogundulika mkoani Dar es salaam ni 60 (42-Kinondoni, 14-Temeke na 4-Ilala) na idadi ya wagonjwa waliopo wodini mpaka sasa ni 13.

Aidha, mlipuko wa ugonjwa huu si mpya hapa nchini kwani uligundulika kwa
mara ya kwanza mnamo Juni 2010 mkoani Dar es Salaam ambapo idadi ya watu 40 walithibitika kuwa na ugonjwa. Pia, kati ya mwezi Mei hadi Julai 2013,wagonjwa 172 walithibitishwa kuugua ugonjwa huu.

Homa ya Dengue

Homa ya dengue ni ugonjwa unaosababishwa na kirusi ambacho kinaenezwa na mbu wa aina ya Aedes.

Dengue in ugonjwa uliosambaa duniani katika nchi za ukanda wa joto. Takribani asilimia 40 ya watu wote duniani wanaishi katika nchi zenye ugonjwa huu. Takwimu za Shirika la Afya Duniani zinathibitisha kuwa takribani matukio milioni 5 ya Dengue yanatolewa taarifa kila mwaka. Watu laki 5 hulazwa hospitali kwa kuathirika na Dengue kali. Homa ya Dengue imeshatokea katika nchi zipatazo 34 barani Afrika.

Hapa Afrika Dengue ni ugonjwa unaojulikana kwa kiwango kidogo sana. Licha ya kwamba milipuko ya kwanza imetokea tangu mwanzoni wa karne ya 19. Matukio ya Ugonjwa huu yameongezeka Afrika tangu miaka ya 1980, matukio mengi yakitokea nchi za ukanda wa Mashariki mwa Afrika ikiwa ni pamoja na Msumbiji, Somalia, Kenya, Komoro, Djibouti na Tanzania. Ikumbukwe kuwa jina “Dengue” linatokana na neno “Dinga” la kiswahili linalolomaanisha ugonjwa unaotakana na pepo yaani Kudinga pepo. Mabaharia wa Kispanish walipokuja kwenye pwani ya Afrika Mashariki walirudi kwao na kuuita “Dengue”.

Dalili za ugonjwa huu ni homa, kuumwa kichwamaumivu ya viungo na uchovu Dalili hizi huanza kujitokeza kuanzia katisiku ya 3 na 14 tangu mtu alipoambukizwa kirusi cha homa ya dengue. Kwa wakati mwinginedalili za ugonjwa huu zinaweza kufanana sana na dalili za malaria, hivyo basi wananchi wanaombwa kuwa wakati wakipata homa kuhakikisha wanapima ili kugundua kama wana vimelea vya malaria ua la ili hatua stahiki zichukuliwe.

Kuna aina 3 tofauti za namna ugonjwa huu unavyoweza kujitokeza iwapo mtu aking`atwa na mbu mwenye virusi hivi;

i.Homa ya dengue (Dengue Febrile Illness): Aina hii huambatanana dalili kuu tatu za homa kali ya ghafla, kuumwa kichwa na maumivu ya viungo au uchovu.Aidha, kwa Tanzania mpaka sasa zaidi ya asilimia 90 ya wagonjwa wamejitokeza na dalili hizi.

ii.Dengue ya damu (Dengue Haemorrhagic Fever): Aina hii yahoma ya dengue huambatana na dalili za mgonjwa kutokwa na damu kwenye fizi au puani, vile vile kutokwa na damu chini ya ngozi.Iwapo mgonjwa huyu ataumia sehemu yoyote ni rahisi kwake kupoteza damu nyingi kupitia kwenye michubuko.

iii.Dengue ya kupoteza fahamu (Dengue Shock syndrome): Aina hii ya homa yadengue huambatana na mgonjwa kupoteza damu nyingi ambayo hupelekea mgonjwakupoteza fahamu. Dalili hizi zimeonekana kwa mgonjwa 1 kati ya wagonjwa 400 waliokwisha kuthibitishwa kuwa na ugonjwa hapa nchini.
 
Kirusi cha homa ya Dengue kinaambukizwa kutoka mtu mmoja hadi mwingine kwa kuumwa na mbu wa Jamii ya Aedes, na hasa Aedes aegypti. Mbu huyu anaishi katika mazingira ya makazi ya binadamu. Huuma wakati ya mchana ndani ya nyumba au kwenye maeneo yenye vivuli, hususani majira ya asubuhi na jioni kabla jua halijazama.

Mbu huyu anazaliana katika maji yaliyotuama hasa kwenye vyombo vya nyumbani, makinga maji ya paa za nyumba, matairi ya gari, ndoo, vikopo, na kadhalika. Kwa bahati mbaya mbu huyu huweza kuzaliana katika vifaa vidogo vidogo ambavyo watu wengi huvidharau. Hivi ni pamoja na makopo ya kuotesha maua, vikombe, vifuu vya nazi, na kadhalika. Majani mapana yanayohifadhi maji ni mazingira mazuri kwa kuzaliana kwa mbu huyu, hivyo maeneo ya bustani siyo ajabu kuwa mahali pazuri kwa mbu hawa.

Ugonjwa huu hauambukizi kwa kumhudumia mgonjwa au kugusa majimaji yanayotoka kwa mgonjwa. Homa ya dengue inaweza kutibika kama mgonjwa atapelekwa hospitali mapema na kupatiwa matibabu ya haraka.Hakuna dawa maalumu ya ugonjwa wala chanjo bali mgonjwa anatibiwa kutokana nadalili zitakazoambatana na ugonjwa huu kama vile homa, kupungukiwa maji au damu. Endapo mgonjwa atachelewa kupatiwa matibabu, mgonjwa anaweza kupoteza maisha.

Jinsi ya kujikinga na ugonjwa wa homa ya dengue

Kuangamiza mazalio ya mbu

  • Fukia madimbwi ya maji yaliyotuamaau nyunyuzia viuatilifu vya kuua viluwiluwivya mbu kwenye madimbwi hayo
  • Ondoa vitu vyote vinavyoweza kuweka mazalio ya mbu kama vile: vifuu vya nazi, makopo, magurudumu ya magari yaliyotupwa hovyo, nk.
  • Fyeka vichaka vilivyo karibu na makazi ya watu
  • Hakikisha maua yandayopandwa kwenye makopo au ndoo hayaruhusu maji kutuama
  • Funika mashimo ya maji takakwa mfuniko imara
  • üSafisha gata za paa la nyumba ili kutoruhusu maji kutuama

Kujikinga na kuumwa na mbu
  • Tumia viuatilifu vya kufukuza mbu “mosquito repellants”
  • Vaa nguo ndefu kujikinga na kuumwa na mbu
  • Tumia vyandarua vilivyosindikwa viuatilifu (kwa wale wanaolala majira ya mchana na hasa kwa watoto)
  • Weka nyavu kwenye madirisha na milango ya nyumba za kuishi


Hatua zinazochukuliwa na Wizara

(i)Hatua za Dharura

Uratibu

  • Timu ya Taifa ya Maafa inayoshirikisha wadau mbalimbali ikiwemo wa Halmashauri za Jiji na Wadau wa Maendeleo hukutana kila mara 2 kwa wiki kutathmini mikakati ya dharura iliyowekwa.
Uelemishaji na Uhamasishaji wa Jamii
  • Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii ilitoa tamko la Serikali kwa nyakati tofauti kuhusu mlipuko wa ugonjwa wa Dengue. Tamko la kwanza lilitolewa kwenye vyombo vya habari tarehe 04 Februari 2014 na Machi 2014.
  • Kuendelea kutoa taarifa ya tahadhari ya ugonjwa huu kupitia kwa Waganga Wakuu wote wa Mikoa na Wilaya kwa Tanzania Bara. Aidha taarifa hii pia iinajumuisha namna mgonjwa anavyoweza kutambuliwa (Ainisho la Ugonjwa), “Ukweli Kuhusu Ugonjwa“(Fact sheet), Mwongozo kwa watumishi wa afya wa namna ya kuchukua sampuli. Vipeperushi vinavyoelezea jinsi ya kujikinga na maambukizi ya ugonjwa huu vitatolewa.
  • Kuendelea kutoa elimu kwa wananchi kupitia Radio, na Runinga. Aidha Wizara kwa kushirikiana na Halmashauri za jiji wameendelea kutumia Maafisa Afyaikiwemo wa kata kuwaelemisha wananchi namna ya kudhibiti ugonjwa kwakutumia vipaza sauti, uongozi wa mitaa

Mafunzo kwa watalaam wa Afya
  • Kuendelea kutoa elimu ya Afya kwa Watumishi wa Afya ikiwa pamoja na madaktari na mafundi maabara namna ya kutambua ugonjwa huu. Aidha watumishi wa hospitali za Muhimbili, Mwananyamala, Amana na Temeke wamekwisha kupewa mafunzo haya na bado wanaendelea kupewa kupitia mikutano yao ya asubuhi (Clinical meetings). Mafunzo haya pia yanaendelea kutolewa kwa vituo vya chini kupitia Halmashauri

Kuimarisha mfumo wa ufuatiliaji na mawasiliano
  • Kuimarisha ufuatiliaji wa ugonjwa huu katika vituo vya kutolea huduma za afya pamoja na mipakani kupitia mfumo wa saveilensi ya Wizara. Aidha, pamoja na Mwongozo huu, Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii imetoa maelekezo kwa Waganga wakuu wa mikoa na wilaya hapa nchini kutoa taarifa za wagonjwa wa Dengue Fever kupitia taarifa za kila juma.
  • Kutoa miongozo ya ufuatiliaji wa ugonjwa huu katika maeneo ya mipakani kuhusu kutokuwepo kwa aina yoyote ya vikwazo vitakavyowekwa kwa ajili kwa wasafiri. Aidha maelekezo hayo yameainisha kuwa iwapo msafiri anayeondoka au kurudi nchini akiwa na dalili tajwa atoe taarifa kwa watumishi wa afya wa mpakani ili hatua stahili ziweze kuchukuliwa
  • Kufuatilia kwa karibu ongezeko la wagonjwa wenye homa isiyo kuwa ya malaria kwa Mikoa na Wilaya zote nchini ili kuweza kufanya uchunguzi wa kina iwapo kuna ugonjwa huu. Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii imeshafanya utafiti mkoani Kagera, Morogoro na Kigoma na kuthibitisha kuwa haijaadhirika na dengue.
  • Kuanzishwa kwa vituo maalum vya ufuatiliaji wa ugonjwa huu katika Hospitali za Manispaa za jiji la Dar es Salaam (Mwananyamala, Amana na Temeke). Aidha, Kituo cha ‘International School of Tanganyika – IST’ kilichopo Manispaa ya Kinondoni na Hospitali ya Taifa ya Muhimbili zinaendelea na ufuatiliaji wa ugonjwa huu. Aidha Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii itafungua pia vituo mkoani Tanga na Mtwara, mikoa imayopakana na nchi jirani yaani Kenya na Msumbiji ambako ugonjwa huu pia umetolewa taarifa.
  • ·Kupeleka taarifa ya mlipuko huu Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO) kama mwongozo wa Kanuni za Afya za Kimataifa uvyaoelekeza.
Upimaji na Tiba
  • Kuimarisha uwezo wa kutambua ugonjwa huu kwa kina kupitia maabara ya Taifa (NHLQATC) iliyopo NIMR. Vile vile Wizara imepeleka vipimo sawia yaani “Dengue Rapid Test Kits” kwa vituo vya Dar es Salaam kuimarisha utambuzi. Vituo hivo ni pamoja na hospitali za Muhimbili, Amana, Mwananyamala, Temeke Hospital, na IST kliniki. Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii imeagiza Bohari Kuu ya Dawa (MSD) kuhakikisha vitendanishi hivi vinakuwepo ili kurahisisha upatikanaji wake kwa Halmashauri zote na kupelekwa kwenye vituo vya chini zaidi. Wizara imeagiza vipimo sawia 750 vya kunyongeza ambavyo tunatarajiwa kuvipata tarehe 22.5.2014
  • Wizara imeweka utaratibu wa kuhakikisha vifaa Tiba vinapatikana wakati wote katika vituo vyote kwa ajili ya kuwahudumia wagonjwa watakaogundulika na kuwa na ugonjwa huu.

Udhibiti wa mbu na mazalia
  • Kudhibiti mbu kupitia kwa kupulizia na kunyunyizia viuatilifu katika baadhi ya maeneo yaliyoathirika katika mkoa wa Dar es salaam ambayo wametoka wagonjwa wengi wa Dengue. Hii inalenga kuangamiza mbu wapevu na viluwiluwi.
Utafiti
Taasisi ya Utafiti ya magonjwa ya Binadamu (NIMR) iko katika maandalizi ya kufanya utafiti kuhusu dengue kwa kuangalia maaeneo makubwa mawili.
  • Ukubwa wa tatizo katika binadamu
  • Mbu waambukizao ugonjwa wa homa ya Dengue- kujua jamii husuka, tabia ya kuuma watu, wapi wanapopendelea kuuma, wapi wanakozaliana kwa wingi na mazingira yao ya kawaida.
Tafiti hizi zinaanzia Dar es Salaam na kuhusisha wilaya zote tatu (Ilala, Kinondoni, Temeke). Tafiti zitaendelea katika baadhi ya mikoa, ikiwa ni pamoja na mikoa 8 ambako vituo vyetu vipo.Takwimu zitakazopatikana zitaboresha mbinu za kupambana na ugonjwa huu

(ii)Hatua za Kudumu

  • WAUJ imeandaa Mpango wa wa namna ya kukabiliana na ugonjwa wa Homa ya Dengue. Mpango huu kwa kushirikisha sekta mbalimbali.
  • Kuimarisha mfumo wa ufuatiliaji wa ugonjwa wa Dengue

Hitimisho

Wananchi wanashauriwa kutokuwa na hofu kuhusu ugonjwa huu kwani hauambukizwi kwa kumhudumia mgonjwa au kwa kugusa majimaji yanayotoka kwa mgonjwa. Hata hivyo tunawashauri wananchi kwenda kwenye vituo vya afya haraka pindi wanonapo dalili za ugonjwa huu.

Mlipuko wa Dengue unadhihirisha kuwa mazingira yetu tunayoishi si salama. Ikumbukwe kuwa, kwa sehemu kubwa, ugonjwa huu unachochewa na mazingira machafu. Aidha mvua hizi kubwa zinazoendelea zonachangia kuongezeka kwa mazalio ya mbu. Utupaji, uzoaji na uhifadhi wa taka katika miji yetu hauridhishi kiasi ambacho kinatoa fursa kwa mazalio ya mbu kuongezeka na hata kuwa karibu zaidi ya makazi ya binadamu.

Kwa kuwa, hadi sasa hakuna chanjo wala dawa maalumu kwa ajili ya kudhibiti au kutibu ugonjwa huu, njia kubwa ya kupambana na ugonjwa huu ni kumzuia binadamu asimwe na mbu. Hivyo basi, mbinu shirikishi za kutokomeza mbu inabidi zitiliwe mkazo katika mapambano dhidi ya homa ya Dengue. Njia bora na rahisi ni kuhakikisha mazalio yote ya mbu yanatokomezwa. Na hili laweza kufanywa na kila mtu kwa nafasi yake.Tunashauri watu wavae nguo zinazofunika mikono na miguu na dawa zinazofukuza mbu (mosquito repellent). Tunaelewa kuwa si kila mtu atakuwa na uwezo wa kununua dawa hizi na ndiyo maana tunakazania swala la kuangamiza mazalia ya mbu ambalo ni jukumu letu wote.Tunaendelea kuhamisisha watu na hasa watoto walale ndani ya vyandarua venye viatilifu wanapolala wakati wa mchana.

Ningependa kuwakumbusha wananchi wa Tanzania kuwa, huu ni muda muafaka wa kuzingatia utunzaji bora wa mazingira yetu. Tukitunza mazingira yetu, nayo yatatutunza na kutuepusha na maradhi yanayoambatana na mazingira machafu.

Charles A. Pallangyo
Katibu Mkuu
12 May 2014