Kanisa lawataka wachungaji wajiuzulu CHADEMA


Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Kusini ambaye pia ni Mchungaji wa Kanisa la Evangelistic Assemblies of God Tanzania (EAGT), Joseph Matare amejiuzulu nafasi yake hiyo kutokana na kanisa lake kuwataka wachungaji wake ambao ni viongozi wa vyama vya siasa kuachana na nafasi zao za kisiasa. 
 
Joseph Matare akizungumza na waandishi wa habari mjini Songea amesema kuwa ameamua kujiuzulu nafasi yake ya uongozi wa Chadema Kanda ya Kusini inayojumuisha mikoa ya Lindi, Mtwara na Ruvuma baada ya kanisa lake katika mkutano wake wa kanda kuagiza wachungaji wake ambao ni viongozi wa siasa kuachia nafasi zao na badala yake wasimamie kazi ya Mungu katika makanisa yao.
 
“Kufuatia maagizo ya mkutano huo wa kanisa uliofanyika Njombe nimeamua kutii... nimeamua kujiuzulu na katibu wangu mkuu, Dk Willibrod Slaa nilimjulisha tangu tarehe 4 Juni mwaka huu,” alisema Matare katika taarifa yake ya kujiuzulu.
 
Amefafanua kuwa muda wa viongozi wa kanda ulikuwa ni wa muda na wa mpito hadi uchaguzi wa kanda utakapopita ambao ulipaswa kufanyika Juni 2014 na kwamba muda umeongezwa hivyo ameona aheshimu maagizo yaliyomweka madarakani.
 
Hata hivyo, Matare anasema kuwa anawatia moyo makamanda wote wa Chadema waliobaki kuendelea kupigania nchi ili iondokane na uovu unaotendeka sasa na kwamba Mungu atakuwa nao wale wote wanaotafuta haki kwa ajili ya wananchi walio wengi.

Rais Kikwete: Uchaguzi Serikali za Mitaa kusogezwa mbele


RAIS Jakaya Kikwete amesema uchaguzi wa serikali za mitaa ambao ulikuwa ufanyike mwezi Oktoba mwaka huu, huenda ukasogezwa mbele kutokana na kutokamilika kwa mchakato wa rasimu ya mabadiliko ya Katiba.
 
Kauli hiyo ameitoa kwenye mkutano wa majumuisho ya ziara yake ya kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo mkoani Tanga.
 
Alisema kulingana na hali ilivyo hivi sasa ambapo Bunge la Katiba halijakamilisha kazi zake, ni dhahiri kwamba uwezekano wa kufanyika kwa uchaguzi huo kwa kutumia Katiba mpya haupo.
 
“Kwa mfano, wabunge endapo wataamua wapitishe kwamba katiba itambue serikali 3 ni lazima kwanza itungwe katiba ya Tanganyika ambayo itaainisha taratibu zitakazotoa mwongozo wa uchaguzi…hata kama itabaki kama ilivyo …. bado muda wa kuandaa huo utaratibu wa uchaguzi wa serikali za mitaa hautatosha kwa sasa”, alisema.
 
Aidha aliongeza, “Nimeona niliseme hili japo kwa ufupi kwamba uchaguzi huu huenda utalazimika kusogezwa mbele kutokana na kutokamilika kwa mchakato wa Rasimu ya mabadiliko ya Katiba“, alisema.
 
Katika hatua nyingine, Rais amewataka Maofisa Kilimo kwenye halmashauri kujiendeleza kitaaluma na kuwa mabingwa waliojikita katika taaluma ya mazao yanayostawi kwenye maeneo yao badala ya kuyashughulikia kwa ujumla mazao yote yanayolimwa na wananchi.
 
Alisema utekelezaji wa agizo hilo utaongeza mavuno kwa zao husika, utapanua wigo wa uzalishaji pamoja na utaalamu katika kushughulikia zao, aina ya zao na kuleta tija katika sekta ya kilimo.
 
Alisema hatua ya maofisa kilimo kuendelea kujishughulisha kwa ujumla na mazao yote yanayostawi bila kuwa na lengo la kusimamia mazao maalumu, kunaifanya sekta hiyo kudumaa na hivyo kushindwa kuwakwamua kiuchumi wananchi.
 
“Nimegundua kwamba watu wetu wengi hawana utaalamu uliobobea…hata maofisa kilimo wetu hawana taaluma maalumu zilizojikita kwenye aina ya mazao mengine zaidi ya mpunga na mahindi, hatua ambayo inawasababisha washindwe kusimamia vizuri uzalishaji wa mazao mengine ambayo yangeweza kuwakwamua kiuchumi wakulima kwenye halmashauri husika,” alisema.
 
Aliongeza, “Kwa hiyo ni jukumu lenu viongozi wa halmashauri kuwachukua maofisa kilimo wenu na kuwapeleka SUA kwa ajili ya ku-specialize (kujikita) kulingana na vipaumbele vyenu vya mazao kwa sababu sio wote wanao ubingwa katika kila zao…tukifanikiwa kwenye hilo tutapata mafanikio zaidi”, alisema.
 
Aidha aliwataka viongozi kwenye mkoa wa Tanga kuhakikisha shughuli za kilimo zinajikita kwenye uzalishaji endelevu wa mazao ya matunda na mboga, kwa kuwa mkoa huo uko katika fursa nzuri kiuzalishaji zaidi ya mazao ya nafaka.

Dayna Nyange asimulia jinsi anavyoshambuliwa na Mashabiki kwa Lugha Chafu baada ya kuamua Kujichubua


Mwimbaji wa kike Dayna Nyange amezungumzia jinsi alivyokutana na changamoto nyingi baada ya kuamua kubadili rangi ya  ngozi yake na kuwa nyeupe.
 
Akiongea katika The Jump Off ya 100.5 Times Fm, Dayna ameeleza kuwa amekuwa akikosolewa na watu wengi huku wengine wakitumia lugha mbaya dhidi yake lakini yeye ameipokea vizuri kwa kuwa anaamini ni watu wanaompenda.
 
“Ni sawa kwa sababu mimi naamini ni watu wangu wa karibu na ni watu ambao wananipenda ndio maana wanakuwa wanasema japo wengine wanatumia kauli mbaya. Lakini pia ni sawa kwa sababu mimi najua hao ni binadamu na kila binadamu anajua jinsi ya kupresent kwa mtu vile ambavyo anajisikia kwa hiyo ni mimi kutumia tu akili nakipokeaje.” Amesema Dayna Nyange.
 
Ameeleza kuwa yeye anaamini hakuna kitu ambacho aliwahi kukifanya kabla kikawa gumzo au tatizo kwa watu na ndio maana watu wanaamua kulichukulia hili kama tatizo kubwa.
 
Mwimbaji huyo alitangaza uamuzi aliouchukua kufuatia changamoto hizo alizokutana nazo ingawa anaamini kila mtu anauhuru wa kufanya maamuzi kama alivyoamua yeye.
 
“Kwa hiyo mimi naweza kusema ni sawa, inawezekana kweli nimekosa. Lakini mimi kama binadamu pia nina maamuzi yangu na nina sababu nyingi tu za kufanya kile ninachokifanya. Japo nimesikia maneno mengi sana mpaka Lol..’nimeacha.!
 
“Siwezi kusema kuwa nimeacha kabisa lakini nimetoka kule nilikokuwa, sasa hivi narudi kuwa Dayna yule ambaye mnataka awe. Japo pia binadamu pia mnakitu kimoja, sifieni kile kilicho bora kabla hakijakuwa sio.” Ameaongeza.

Rose Ndauka Amkimbia Mumewe


Staa wa filamu za Kibongo, Rose Ndauka hivi karibuni aliamua kumkimbia mumewe Malick Bandawe, kisa mfungo wa Ramadhani ambapo sasa anaishi Kigogo na mama yake mzazi. 

Akipiga stori na mwanahabari wetu, Rose alisema amelazimika kwenda nyumbani kwao ili kumpisha mumewe atimize nguzo hiyo ya Uislam bila kipingamizi kutokana na kutokufunga ndoa.
 
“Mimi sifungi hivyo nimeona pia ni jambo la busara kumpa nafasi mwenzangu kwa ajili ya kufanya ibada hiyo, mwezi ukiisha nitarudi na maisha yetu yataendelea kama kawaida,” alisema Rose ambaye awali alikuwa akiishi na mumewe huyo Tandale jijini Dar.

Mwanamke Aliyemng'ata Hausigeli na kumchoma Pasi Aachiwa


Mtuhumiwa wa kesi ya kujeruhi kwa kumng'ata sehemu mbalimbali za mwili  mfanyakazi wa ndani, inayomkabili Amina Maige (42) amepatiwa dhamana jana baada  ya mahakama kuthibitisha kuwa hasira kutoka kwa wananchi zimepungua.
 
Hakimu wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kinondoni, Yohana Yongolo alisema ameridhishwa na ufafanuzi uliotolewa na Mwendesha mashitaka wa Serikali pamoja na Wakili wa mshitakiwa kuwa haki ya dhamana itolewe kwa kufuata masharti na kwamba hakuna uhalifu wowote utakaofanyika dhidi ya mshitakiwa huyo.
 
Hakimu  Yongolo alitoa masharti ya dhamana ambayo yalimtaka Maige kutoondoka nje ya Dar es salaam bila ya ruhusa ya mahakama hiyo.
 
Pia alitoa masharti ya kuwa na wadhamini wawili wa kuaminiwa kutoka taasisi inayotambulika hapa nchini ambapo mdhamini huyo anaweza kuwa mwajiriwa, mfanya biashara na mkulima.
 
Alisema wadhamini hao watatakiwa kusaini hati ya makubaliano kwa kila mmoja kulipa Sh milioni tatu.
 
Aliongeza kuwa kesi hiyo itasikilizwa Julai 22 mwaka huu.
 
Maige alidaiwa Januari mwaka jana hadi Juni mwaka huu, alimng'ata na kumchoma na  pasi  sehemu mbalimbali za mwili wa  mfanyakazi waje wa ndani Yusta Kashinde (20) na kumsababishia maumivu mwilini.

Mbio za Urais 2015: Fredrick Sumaye Asema yeye ndo Tumaini pekee la Watanzania


WAZIRI Mkuu Mstaafu, Fredrick Sumaye, amesema yeye ni tumaini la Watanzania na mpambanaji wa vita dhidi ya maovu.
 
Kutokana na hali hiyo, amesema ni jemadari hodari aliyeungana na askari wapiganaji hodari wa vita ambao wataleta ushindi usio na shaka.
 
Kauli hiyo aliitoa jijini Mwanza jana, katika hotuba yake ya uzinduzi wa taasisi ya Vijana ya Tanzania Youth (TYDC), ambako alipinga hatua ya baadhi ya wanasiasa kununua wapiga kura kwenye uchaguzi na kufanikisha kitendo hicho ni sawa na uroho wa  madaraka. 
 
Alisema hali hiyo ni hatari, kwani wanasiasa wa aina hiyo wanapaswa kuangaliwa kwa umakini wa hali ya juu, wanaweza kulisambaratisha Taifa.
 
Sumaye ni mmoja wa makada sita wa CCM waliopewa onyo kutokana na kile kilichoelezwa kuanza kampeni za kuwania urais kabla ya wakati.
 
Akizungumza na MTANZANIA baada ya uzinduzi wa taasisi hiyo, Sumaye alisema yupo tayari kugombea urais iwapo ataombwa kufanya hivyo.
 
Akijibu maswali kwa waandishi wa habari, alisema dhamira yake katika kujitosa kuwania urais ipo, lakini pale atakapoombwa kugombea.
 
“Nikiombwa kugombea urais nitagombea, hilo wala halina tatizo…na mjue kutangaza nia siyo kosa kwa mujibu wa kanuni za CCM, ila kosa ni kufanya kampeni kabla ya muda, wakati rais anapomaliza muda wake wagombea wengi hujitokeza kuwania nafasi hiyo, sasa hata mimi nikiombwa nitagombea,” alisema Sumaye.
 
Sumaye, anayetajwa kuwa miongoni mwa wanasiasa ndani ya CCM wanaotaka kuwania urais mwaka 2015, akizungumza katika uzinduzi huo wa TYDC, alisema kuna watu wamekuwa wakitumia nguvu ya fedha kusaka madaraka na kuwafananisha na watu wafupi wanalazimisha kupanda juu ya stuli ili waonekane mbele ya jamii kwa kutumia nguvu kubwa ya fedha.
 
Alisema watu hao ni hatari iwapo wakichaguliwa na kushuka juu ya stuli kwa vile hawataonekana tena kuwasaidia wananchi na kubainisha wamekuwa wakiwatumia vijana vibaya ili kukidhi malengo yao binafsi, yakiwemo ya kisiasa.
 
Katika kongamano hilo, Sumaye alitangaza kuwa mlezi wa vijana nchini na kuwaahidi maisha ya matumaini kwa miaka ijayo.
 
“Mimi nataka niwe mlezi wa vijana wa Tanzania nzima ili wawe na maisha ya matumaini. Ninyi vijana mtu akiwaleteeni hela chukueni kuleni halafu mnamchagua mwingine. Yaani hata Sumaye akileta msikatae hela, chukueni kuleni msimchague, maana mtu anayetumia nguvu ya fedha kusaka madaraka ya Serikali za Mitaa, udiwani, ubunge na hata urais huyo hafai na ni dhaifu,” alisema Sumaye, huku akieleza hakuja kwenye kongamano hilo kwa sababu za kisiasa.
 
Aliwaasa vijana wote, hususan waliopo masomoni wasidanganyike wala kutegemea kupata ajira za ofisini na kwamba wasiopata ajira wasikubali kutumiwa kisiasa, vijana watakaotumiwa watakuwa wamejiunga katika kundi la wala rushwa na wapokea rushwa, watakuwa wamejiunga kwenye kundi la mafisadi na la maangamizi kwa taifa.
 
Alisema kwamba vijana ni jeshi muhimu la taifa kwa maslahi ya taifa na wananchi wake na siyo jeshi la kuleta maafa katika jamii, hivyo atakuwa mlezi wa vijana kwa mambo yote na sifa anayoipenda ni mtu kuwa mzalendo wa kweli, kusimamia haki ya umma na siyo maslahi binafsi.
 
Alisema kwamba, hivi sasa Watanzania wanaelekea kwenye uchaguzi na fedha nyingi zinatembezwa kwa vijana ili watoa rushwa wachaguliwe katika nafasi wanazoomba na kudai siku hizi kumeibuka mtindo wa watoa fedha kuitwa wakarimu na wasiotoa kuhonga wao huitwa wachoyo.
 
“Mliponitaka niwe mlezi wenu nilikubali kwa sababu mimi ni mpambanaji wa vita dhidi ya matatizo na maovu hayo ambayo TYDC imeyaweka kama malengo yake makuu.
 
“Hivyo niliona nimepata wapiganaji wenzangu katika vita hii na kwa bahati nzuri wapiganaji wenyewe ni vijana ambao ni wengi, ni wenye nguvu na ndio wenye uchungu na nchi yao. 
"Mimi ninawaahidi kuwa mmempata jemadari hodari wa kuongoza vita hii na yeye jemadari amepata askari mashujaa wa kupigana vita hiyo,” alisema.
 
Alisema muunganiko huo wa wawili wa jemadari hodari na askari wapiganaji hodari wa vita utaleta ushindi usio na shaka.
 
“Kama unavyoambiwa wewe na wenzako wengine wasiokuwa na mahesabu nao huambiwa vivyo hivyo. Lakini la msingi ujue kuwa kama mtu anatumia njia hizo za mkato kutaka kuingia madarakani, huyo mtu hajiamini na wala hana uhakika na uwezo wake wa kumudu hayo madaraka anayoyatafuta, vinginevyo asingehangaika kuhonga watu,” alisema Sumaye.
 
Awali akimkaribisha Sumaye kuzungumza na halaiki ya vijana zaidi ya 300, Mwenyekiti wa TYDC, Lengai Thomas Ole Sabaya, alionekana wazi kumpigia ‘debe’ Sumaye katika harakati zake za kisiasa, kwa kusema wakati wa utawala wake na Mkapa fedha ya Tanzania ilikuwa na thamani kuliko ilivyo leo hii.
 
Sumaye alikuwa Waziri Mkuu kwa miaka 10 katika Serikali ya Rais Benjamin Mkapa.
Februari 18, mwaka huu, Chama Cha Mapinduzi (CCM), kupitia Kamati Ndogo ya Udhibiti na Nidhamu katika kikao chake ilipendekeza kuchukuliwa hatua za kinidhamu kwa makada wake ambao wameanza kampeni ya kuwania urais wa mwaka 2015.
 
Uamuzi huo wa kamati hiyo ya maadili ulibarikiwa na Kamati Kuu (CC) ya CCM, iliyokutana Februari 17, mwaka huu mjini Dodoma, chini ya Mwenyekiti wake, Rais Jakaya Kikwete.
 
Makada waliopewa adhabu ya mwaka mmoja kwa tuhuma za kuanza kampeni za kuwania urais kabla ya wakati ni January Makamba, Waziri Mkuu wa zamani Edward Lowassa, Waziri Mkuu Mstaafu Frederick Sumaye, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe.
 
Wengine ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Uhusiano na Uratibu) Steven Wassira pamoja na aliyewahi kuwa Waziri wa Nishati na Madini ambaye ni Mbunge wa Sengerema, William Ngeleja.
 
Katika adhabu hiyo, makada hao walizuiwa kujihusisha na masuala ya kisiasa ndani ya chama hicho kwa miezi 12, huku mwenendo wao wa kisiasa ukifuatiliwa chini ya uangalizi mkali katika kipindi chote cha kutumikia adhabu hiyo.
 
Kabla ya adhabu hiyo, makada hao waliitwa na kuhojiwa na Kamati Ndogo ya Maadili ambayo iliwatia hatiani kwa kutumia Kitabu cha Kanuni ya Uongozi na Maadili ya CCM, toleo la Februari 2010, Ibara 6 (7)(i).

Credit: Mtanzania

VJ Penny Achumbiwa.....Sasa kuanza Maisha Mapya baada ya kutemana na Diamond


Mtangazaji maarufu nchini VJ Penny ambaye alikuwa mpenzi wa Diamond Platnumz amechumbiwa.  Kupitia Instagram Penny ameweka picha akiwa amevaa pete ya uchumba  na  kuandika  ujumbe  huu: “Road trip ….site her we come…cc @halimakimwana1.” 
Pia juzi  tulisikia   kuwa Penny amechumbiwa ingawa hatukupata habari kwa kina mpaka Penny mwenyewe alipoweka picha Instagram  akiwa  amevaa  pete  ya  Uchumba.

VJ Penny ambaye  inadaiwa alikuwa chaguo la kwanza la mama Diamond Platinumz ameweka picha hiyo siku moja baada ya Wema Sepetu kupost picha nyingi kwenye Instagram akiwa na mama Diamond kwenye sherehe ya siku yake ya kuzaliwa na kuzipa caption mbalimbali huku nyingine zikiwa na vijembe.
Tunampa hongera zote VJ Penny kwa  kuchumbiwa.