Mahakama ya Hakimu Mkazi Kinondoni, Dar es Salaam imeweka kibano kwa watu wenye mavazi yasiyo na staha kuingia makahamani hapo kwa kuwazuia mlangoni.
Miongoni
mwa mavazi ambayo akivaa mtu anazuiwa kuingia si tu ndani ya vyumba vya
Mahakama, bali pia kwenye viwanja vyake, ni yanayobana, yanayoacha
mgongo wazi, fupi na mashati au blauzi za mikono mifupi.
Hatua
hiyo ilianza kutekelezwa takribani wiki tatu zilizopita. Kibano hicho
kinamuhusu mtu yeyote mwenye shughuli mahakamani hapo wakiwemo
mashahidi, wasikilizaji wa kesi na wanahohitaji huduma mbalimbali.
Hakimu
Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Kweyi Rusemwa aliliambia gazeti hili jana
Dar es Salaam kuwa mavazi hayo yanashusha heshima na hivyo watahakikisha
wanaofika mahakamani hapo wanabadilika kimtazamo.
“Kama
mtu anakuja kwa ajili ya Mahakama lazima avae mavazi ambayo si kero kwa
mwingine. Wanaofika hapa wakiwa na mavazi yasiyostahili wataishia
nje,’’ alisema Rusemwa.
Alitahadharisha
anayefika mahakamani kuwa na khanga ili akibainika vazi alilovaa
halistahili, aweze kujisitiri kwa kufunga khanga hiyo na kuingia
mahakamani kupata huduma.
Alisema
tatizo la mavazi yasiyostahili limekuwa kubwa hususani miongoni mwa
wanawake ambao baadhi hawatambui thamani yao kwa kuamua kuvaa mavazi
yasiyo na heshima.
Hata hivyo, alisema kwa upande wa washitakiwa, ipo changamoto kubwa kwao katika kudhibiti uvaaji usiofaa.
Alitoa
mfano wa watu wanaofikishwa mahakamani kwa mashitaka ya kuuza miili
yao, kwamba wengi hukamatwa wakiwa nusu uchi na kwamba inapotokea
wakafikishwa mahakamani, hushindwa kuwarudisha.
Mwandishi
wa habari hii alishuhudia baadhi ya wanawake waliorudishwa langoni
ambao baadhi walikuwa wakihaha kuomba khanga ili waruhusiwe kuingia
mahakamani.
Pamoja
na walinzi kudhibiti mavazi hayo mlangoni, vile vile matangazo
yamewekwa kuelekeza wageni wanaofika hapo kuzingatia masharti hayo ya
uvaaji.