Mfanyakazi wa ndani, miaka 14 mkazi wa kijiji cha Mdenge, Kata ya Likombe katika Wilaya ya Mtwara, amebakwa na mwajiri wake usiku wa kuamkia jana na kumsababishia maumivu makali na kisha kutokomea kusikojulikana.
Akiongea na FikraPevu jana Jumatatu Juni 16, 2014, Mama mzazi wa mtoto huyo, mwenye umri wa miaka 36, amesema mtoto wake amekumbana na masahibu hayo siku nne tangu aanze kufanya kazi kwa mwajiri wake aliyemtaja kwa jina moja la, Sharifu (42), mfanyakazi katika kiwanda cha kuzalisha saruji cha Alosko mkoani humo.
Amebainisha kuwa, mtoto wake alipata kazi ya kufanya kazi za ndani kwa mwajiri huyo Juni 12, 2014 ambapo ilipofikia usiku wa kuamkia leo mtoto huyo aliamua kutoroka nyumbani kwa mwajiri wake anayeishi na mke wake bila kuaga kutokana na hofu ya kuzuiwa kwenda kwao au kufanyiwa unyama zaidi na kukimbilia nyumbani kwao.
“Alivyopata kazi anasema hii sio mara ya kwanza kufanyiwa hivyo hii ni mara ya pili, usiku wa kuamkia Jumamosi ya Juni 14, 2014 alimuingilia mtoto wangu na alipomwambia atatoa taarifa akamwambia asiseme kwa mtu yeyote kwani atamfanya kama mtoto wake, sasa leo tena amemuingilia.
"Nimemkuta yule mama aliyekuwa anafanya kazi kwake amesema alihisi kuwa kuna huo mchezo lakini aliogopa kuniambia tangu Jumamosi” alisema mama wa mtoto.
Kwa upande wa mtoto huyo, amesema ,“Nilikuwa nimelala usiku wa manane ndipo niliposhtuka, nilipotaka kupiga kelele alinikataza kuwa nisiseme kwa mtu kwani atanifanya kama mtoto wake, na usiku wa kuamkia leo alikuwa ameenda kuangalia mpira nilivyoshtuka alikuwa ameniingilia kimwili ndio nikaondoka asubuhi kwenda kwetu kwa maana alisema nisipige kelele”
Taarifa yatolewa Polisi
Mama mzazi wa mtoto huyo amesema wameripoti tukio hilo katika Kituo cha Polisi Mtwara, kwa tuhuma hizo na amefunguliwa jalada namba Mt/RB/2198/2014 ambapo mtoto huyo amefanyiwa vipimo katika kituo cha Polisi kilichopo wilayani humo na kugundulika kuwa alibakwa na kupata majeraha makubwa.
FikraPevu ilimtafuta Kamanda wa Polisi wa mkoani humo, Zelothe Stephen, ambaye hakupatikana kupitia simu yake ya mkoni baada ya kuita bila kupokelewa, huku upande wa ndugu wa mtuhumiwa wakigoma kuongelea suala hilo wakidai hawajui alipo ndugu yao licha ya kushangazwa na tukio hilo.
Chanzo: Fikra Pevu