Wanaovaa Vibaya marufuku Mahakamani Kinondoni......Mavazi ambayo hayatakiwi ni Vimini,yanayobana, yanayoacha mgogo wazi na mengine


Mahakama ya Hakimu Mkazi Kinondoni, Dar es Salaam imeweka kibano kwa watu wenye mavazi yasiyo na staha kuingia makahamani hapo kwa kuwazuia mlangoni. 
 
Miongoni mwa mavazi ambayo akivaa mtu anazuiwa kuingia si tu ndani ya vyumba vya Mahakama, bali pia kwenye viwanja vyake, ni yanayobana, yanayoacha mgongo wazi, fupi na mashati au blauzi za mikono mifupi. 
 
Hatua hiyo ilianza kutekelezwa takribani wiki tatu zilizopita. Kibano hicho kinamuhusu mtu yeyote mwenye shughuli mahakamani hapo wakiwemo mashahidi, wasikilizaji wa kesi na wanahohitaji huduma mbalimbali. 
 
Hakimu Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Kweyi Rusemwa aliliambia gazeti hili jana Dar es Salaam kuwa mavazi hayo yanashusha heshima na hivyo watahakikisha wanaofika mahakamani hapo wanabadilika kimtazamo.
 
“Kama mtu anakuja kwa ajili ya Mahakama lazima avae mavazi ambayo si kero kwa mwingine. Wanaofika hapa wakiwa na mavazi yasiyostahili wataishia nje,’’ alisema Rusemwa.
 
Alitahadharisha anayefika mahakamani kuwa na khanga ili akibainika vazi alilovaa halistahili, aweze kujisitiri kwa kufunga khanga hiyo na kuingia mahakamani kupata huduma. 
 
Alisema tatizo la mavazi yasiyostahili limekuwa kubwa hususani miongoni mwa wanawake ambao baadhi hawatambui thamani yao kwa kuamua kuvaa mavazi yasiyo na heshima.
 
Hata hivyo, alisema kwa upande wa washitakiwa, ipo changamoto kubwa kwao katika kudhibiti uvaaji usiofaa. 
 
Alitoa mfano wa watu wanaofikishwa mahakamani kwa mashitaka ya kuuza miili yao, kwamba wengi hukamatwa wakiwa nusu uchi na kwamba inapotokea wakafikishwa mahakamani, hushindwa kuwarudisha. 
 
Mwandishi wa habari hii alishuhudia baadhi ya wanawake waliorudishwa langoni ambao baadhi walikuwa wakihaha kuomba khanga ili waruhusiwe kuingia mahakamani.
 
Pamoja na walinzi kudhibiti mavazi hayo mlangoni, vile vile matangazo yamewekwa kuelekeza wageni wanaofika hapo kuzingatia masharti hayo ya uvaaji.