Tabora: Walimu 298 walala sakafuni kwa siku 4 kufuatilia mishahara Igunga.......Hawajalipwa mishahara tangu mwezi Aprili

Walimu  wakiwa wamelala sakafuni katika ofisi za halmashauri.

JUMLA ya Walimu 298 wa shule za msingi na sekondari walioajiriwa mwaka huu Wilayani Igunga mkoani Tabora, wameendelea na mgomo wa kubaki katika na kulazimika kulala katika viti na meza katika ukumbi wa Halmashauri hiyo siku nne mfululizo wakishinikiza serikali ya Wilaya ya Igunga kuwalipa mishahara yao.

Wakizungumza na FikraPevu leo Jumatatu Juni 16, 2014 baadhi yao wakiwa na watoto wachanga wamelalamikia maisha magumu wanayolazimika kuishi kwa kuomba omba kufuatia serikali ya Wilaya kushindwa kuwalipa mishahara yao tangu mwezi Aprili mwaka huu, na serikali ya Wilaya hiyo kuwa na kauli tata kwa kile wanachodai ni kuwadanganya kuwa wangewalipa fedha zao Juni 13, mwaka huu agizo ambalo uongozi wa Wilaya hiyo lakini leo wanadaiwa kulitupilia mbali.

Aidha, wamesema tamko lililotolewa na Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, Rustica Turuka kuwa wangelipwa fedha kutokana na mapato yatokanayo na makusanyo ya Halmashauri hiyo, lakini leo wamelitupilia mbali tamko hilo kwa kuwapiga danadana kuwa fedha hazitoki katikahalmashauri hiyo bali zinatoka hazina.

Baadhi ya waalimu hao, Joseph Ndonga, amesema wamekubaliana kwa pamoja na kusisitiza kuwa wataendelea kuishi katika ukumbi wa halmashauri hadi malipo yao yatakapofanyika, kwani baadhi yao wamefukuzwa kwenye nyumba zo walizopanga kutokana na kushindwa kulipa kodi ya nyumba.

“Hapa tulipo ni siku ya nne kuanzia Ijumaa Juni 13, 2014, tutaendelea kuwabana hadi watupe hela zetu kwamaana sisi maeneo tunayoishi tunakabiliwa na ukata wa hela umekopa unajua mwisho wa mwezi unapata hela lakini hadi sasa hawasikilizi kilio chetu tumeitwa na DED kuwa tukubali kupokea shilingi laki moja tumeikataa kwamaana sio hela tunayodai”  alisema Ndonga

Kaimu Afisa Utumishi wa Halmashauri hiyo, Fredi Mhecho, amesema kuwa sababu ya kucheleweshwa malipo ya waalimu hao ni zoezi la kuhakiki majina kuendeshwa kwa awamu na kuanzia Aprili hadi mwezi huu zoezi hilo bado linaendelea na hadi sasa bado wanajaribu kuangalia namna ya kutatua tatizo hilo.

Polisi wazingira eneo walilopo walimu
Katika hali ya kushangaza walimu hao wamedai kuzungukwa na Askari wa kikosi cha kutuliza ghasia (FFU) mjini humo, hali ambayo imetajwa kuwafanya baadhi ya walimu hao kuingiwa na hofu baada ya kusimamia msimamo wa kutoondoka katika ukumbi wa Halmashauri hiyo.

“Wakuu wa idara wamepiga simu Polisi kuomba msaada ili waweze kutuondoa hapa gari la Polisi liko hapa na polisi wa Kikosi Kutuliza ghasia (FFU) wapo na mabomu ya machozi wakiwa wanazunguka katika maeneo tuliyopo” alikaririwa mmoja wa walimu hao.

Kamanda wa Polisi mkoani humo, Susan Kaganda, amesema “Hakuna Polisi waliopo katika ukumbi wa Halmashauri, ninachojua waalimu wapo pale tangu Ijumaa hadi leo lakini kwa upande wa Polisi kuwepo katika hilo eneo hakuna”.

Tafiti zinaonyesha kuwa, walimu wa shule za msingi na sekondari mkoani humo wakati mwingine hulazimika kuacha kufundisha kutokana na tatizo la ukosefu wa maji kiasi cha kuwalazimu kwenda kutafuta huduma hiyo kwa muda mrefu bila kuingia darasani.

 
Polisi  wakiwa  wamezingira  eneo  hilo.

 Chanzo: Fikra  Pevu