WAZIRI Mkuu Mstaafu, Fredrick Sumaye, amesema yeye ni tumaini la Watanzania na mpambanaji wa vita dhidi ya maovu.
Kutokana na hali hiyo, amesema ni jemadari hodari aliyeungana na
askari wapiganaji hodari wa vita ambao wataleta ushindi usio na shaka.
Kauli hiyo aliitoa jijini Mwanza jana, katika hotuba yake ya uzinduzi
wa taasisi ya Vijana ya Tanzania Youth (TYDC), ambako alipinga hatua ya
baadhi ya wanasiasa kununua wapiga kura kwenye uchaguzi na kufanikisha
kitendo hicho ni sawa na uroho wa madaraka.
Alisema hali hiyo ni hatari, kwani wanasiasa wa aina hiyo wanapaswa
kuangaliwa kwa umakini wa hali ya juu, wanaweza kulisambaratisha Taifa.
Sumaye ni mmoja wa makada sita wa CCM waliopewa onyo kutokana na kile
kilichoelezwa kuanza kampeni za kuwania urais kabla ya wakati.
Akizungumza na MTANZANIA baada ya uzinduzi wa taasisi hiyo, Sumaye
alisema yupo tayari kugombea urais iwapo ataombwa kufanya hivyo.
Akijibu maswali kwa waandishi wa habari, alisema dhamira yake katika
kujitosa kuwania urais ipo, lakini pale atakapoombwa kugombea.
“Nikiombwa kugombea urais nitagombea, hilo wala halina tatizo…na mjue
kutangaza nia siyo kosa kwa mujibu wa kanuni za CCM, ila kosa ni
kufanya kampeni kabla ya muda, wakati rais anapomaliza muda wake
wagombea wengi hujitokeza kuwania nafasi hiyo, sasa hata mimi nikiombwa
nitagombea,” alisema Sumaye.
Sumaye, anayetajwa kuwa miongoni mwa wanasiasa ndani ya CCM wanaotaka
kuwania urais mwaka 2015, akizungumza katika uzinduzi huo wa TYDC,
alisema kuna watu wamekuwa wakitumia nguvu ya fedha kusaka madaraka na
kuwafananisha na watu wafupi wanalazimisha kupanda juu ya stuli ili
waonekane mbele ya jamii kwa kutumia nguvu kubwa ya fedha.
Alisema watu hao ni hatari iwapo wakichaguliwa na kushuka juu ya
stuli kwa vile hawataonekana tena kuwasaidia wananchi na kubainisha
wamekuwa wakiwatumia vijana vibaya ili kukidhi malengo yao binafsi,
yakiwemo ya kisiasa.
Katika kongamano hilo, Sumaye alitangaza kuwa mlezi wa vijana nchini na kuwaahidi maisha ya matumaini kwa miaka ijayo.
“Mimi nataka niwe mlezi wa vijana wa Tanzania nzima ili wawe na
maisha ya matumaini. Ninyi vijana mtu akiwaleteeni hela chukueni kuleni
halafu mnamchagua mwingine. Yaani hata Sumaye akileta msikatae hela,
chukueni kuleni msimchague, maana mtu anayetumia nguvu ya fedha kusaka
madaraka ya Serikali za Mitaa, udiwani, ubunge na hata urais huyo hafai
na ni dhaifu,” alisema Sumaye, huku akieleza hakuja kwenye kongamano
hilo kwa sababu za kisiasa.
Aliwaasa vijana wote, hususan waliopo masomoni wasidanganyike wala
kutegemea kupata ajira za ofisini na kwamba wasiopata ajira wasikubali
kutumiwa kisiasa, vijana watakaotumiwa watakuwa wamejiunga katika kundi
la wala rushwa na wapokea rushwa, watakuwa wamejiunga kwenye kundi la
mafisadi na la maangamizi kwa taifa.
Alisema kwamba vijana ni jeshi muhimu la taifa kwa maslahi ya taifa
na wananchi wake na siyo jeshi la kuleta maafa katika jamii, hivyo
atakuwa mlezi wa vijana kwa mambo yote na sifa anayoipenda ni mtu kuwa
mzalendo wa kweli, kusimamia haki ya umma na siyo maslahi binafsi.
Alisema kwamba, hivi sasa Watanzania wanaelekea kwenye uchaguzi na
fedha nyingi zinatembezwa kwa vijana ili watoa rushwa wachaguliwe katika
nafasi wanazoomba na kudai siku hizi kumeibuka mtindo wa watoa fedha
kuitwa wakarimu na wasiotoa kuhonga wao huitwa wachoyo.
“Mliponitaka niwe mlezi wenu nilikubali kwa sababu mimi ni mpambanaji
wa vita dhidi ya matatizo na maovu hayo ambayo TYDC imeyaweka kama
malengo yake makuu.
“Hivyo niliona nimepata wapiganaji wenzangu katika vita hii na kwa
bahati nzuri wapiganaji wenyewe ni vijana ambao ni wengi, ni wenye nguvu
na ndio wenye uchungu na nchi yao.
"Mimi ninawaahidi kuwa mmempata
jemadari hodari wa kuongoza vita hii na yeye jemadari amepata askari
mashujaa wa kupigana vita hiyo,” alisema.
Alisema muunganiko huo wa wawili wa jemadari hodari na askari wapiganaji hodari wa vita utaleta ushindi usio na shaka.
“Kama unavyoambiwa wewe na wenzako wengine wasiokuwa na mahesabu nao
huambiwa vivyo hivyo. Lakini la msingi ujue kuwa kama mtu anatumia njia
hizo za mkato kutaka kuingia madarakani, huyo mtu hajiamini na wala hana
uhakika na uwezo wake wa kumudu hayo madaraka anayoyatafuta, vinginevyo
asingehangaika kuhonga watu,” alisema Sumaye.
Awali akimkaribisha Sumaye kuzungumza na halaiki ya vijana zaidi ya
300, Mwenyekiti wa TYDC, Lengai Thomas Ole Sabaya, alionekana wazi
kumpigia ‘debe’ Sumaye katika harakati zake za kisiasa, kwa kusema
wakati wa utawala wake na Mkapa fedha ya Tanzania ilikuwa na thamani
kuliko ilivyo leo hii.
Sumaye alikuwa Waziri Mkuu kwa miaka 10 katika Serikali ya Rais Benjamin Mkapa.
Februari 18, mwaka huu, Chama Cha Mapinduzi (CCM), kupitia Kamati
Ndogo ya Udhibiti na Nidhamu katika kikao chake ilipendekeza kuchukuliwa
hatua za kinidhamu kwa makada wake ambao wameanza kampeni ya kuwania
urais wa mwaka 2015.
Uamuzi huo wa kamati hiyo ya maadili ulibarikiwa na Kamati Kuu (CC)
ya CCM, iliyokutana Februari 17, mwaka huu mjini Dodoma, chini ya
Mwenyekiti wake, Rais Jakaya Kikwete.
Makada waliopewa adhabu ya mwaka mmoja kwa tuhuma za kuanza kampeni
za kuwania urais kabla ya wakati ni January Makamba, Waziri Mkuu wa
zamani Edward Lowassa, Waziri Mkuu Mstaafu Frederick Sumaye, Waziri wa
Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe.
Wengine ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Uhusiano na Uratibu) Steven
Wassira pamoja na aliyewahi kuwa Waziri wa Nishati na Madini ambaye ni
Mbunge wa Sengerema, William Ngeleja.
Katika adhabu hiyo, makada hao walizuiwa kujihusisha na masuala ya
kisiasa ndani ya chama hicho kwa miezi 12, huku mwenendo wao wa kisiasa
ukifuatiliwa chini ya uangalizi mkali katika kipindi chote cha kutumikia
adhabu hiyo.
Kabla ya adhabu hiyo, makada hao waliitwa na kuhojiwa na Kamati Ndogo
ya Maadili ambayo iliwatia hatiani kwa kutumia Kitabu cha Kanuni ya
Uongozi na Maadili ya CCM, toleo la Februari 2010, Ibara 6 (7)(i).
Credit: Mtanzania