Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Kusini ambaye pia ni Mchungaji wa Kanisa la Evangelistic Assemblies of God Tanzania (EAGT), Joseph Matare amejiuzulu nafasi yake hiyo kutokana na kanisa lake kuwataka wachungaji wake ambao ni viongozi wa vyama vya siasa kuachana na nafasi zao za kisiasa.
Joseph Matare akizungumza na waandishi wa habari
mjini Songea amesema kuwa ameamua kujiuzulu nafasi yake ya uongozi wa
Chadema Kanda ya Kusini inayojumuisha mikoa ya Lindi, Mtwara na Ruvuma
baada ya kanisa lake katika mkutano wake wa kanda kuagiza wachungaji
wake ambao ni viongozi wa siasa kuachia nafasi zao na badala yake
wasimamie kazi ya Mungu katika makanisa yao.
“Kufuatia maagizo ya mkutano huo wa kanisa
uliofanyika Njombe nimeamua kutii... nimeamua kujiuzulu na katibu wangu
mkuu, Dk Willibrod Slaa nilimjulisha tangu tarehe 4 Juni mwaka huu,”
alisema Matare katika taarifa yake ya kujiuzulu.
Amefafanua kuwa muda wa viongozi wa kanda ulikuwa
ni wa muda na wa mpito hadi uchaguzi wa kanda utakapopita ambao ulipaswa
kufanyika Juni 2014 na kwamba muda umeongezwa hivyo ameona aheshimu
maagizo yaliyomweka madarakani.
Hata hivyo, Matare anasema kuwa anawatia moyo
makamanda wote wa Chadema waliobaki kuendelea kupigania nchi ili
iondokane na uovu unaotendeka sasa na kwamba Mungu atakuwa nao wale wote
wanaotafuta haki kwa ajili ya wananchi walio wengi.