KOCHA WA TOTO AFRICANS AWAAGA RASMI WACHEZAJI NA WAKAZI WA JIJI LA MWANZA

 Kocha mkuu wa timu ya Toto Africans mjerumani Martin Grelics jana amewaaga wachezaji na mashabiki wa Toto African mara baada ya mchezo kati ya Toto Africans dhidi ya Mgambo Shooting ambao ulimalizika kwa Toto kuibuka na ushisndi wa goli 1-0.

Grelics amesema huo ndio ulikuwa mchezo wake wa mwisho yeye kuifundisha Toto kama kocha mkuu na tayari ameshabwaga manyanga na akatumia fursa hiyo kuwaaga wachezaji wake na mashabiki wakati akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kumalizika kwa mchezo kwenye uwanja wa CCM Kirumba, jijini Mwanza.

“Huu ulikuwa ni mchezo wangu wa mwisho nikiwa kwenye jiji zuri la Mwanza, najisikia vibaya kuondoka kwenye jiji hili lakini kama nilivyowaambia wiki iliyopita inabidi niondoke”, alisema Grelics baada ya kuzungumzia mchezo kati ya Toto Africa dhidi ya Mgambo Shooting.

Wiki iliyopita Grelics aliuandikia barua uongozi wa timu ya Toto Africans ya kujiuzulu nafasi ya ukocha mkuu kutokana na timu hiyo kuwa na mgogoro na wachezaji hali iliyopelekea wachezaji kugoma kufanya mazoezi kwa ajili ya michezo ya ligi iliyokuwa mbele yao wakidai pesa za mishahara na posho zao.

Toto Africans imecheza mechi tisa, imeshinda mechi tatu, imetoka sare michezo minne na kupoteza mechi mbili huku ikishikilia nafasi ya nane kati ya timu 16 kwenye msimamo wa ligi kuu ya VodacomTanzania bara