BINTI aliyejaliwa uzuri wa sura anayeng’ara kwenye filamu za Kibongo, anamshawishi mumewe Hamad Ndikumana aje kucheza Yanga ya chini ya kocha, Marcio Maximo.
Ndikumana ambaye kwa sasa anaichezea Vital’o ya
Bujumbura, Burundi ameweka wazi kwamba binti huyo, Irene Uwoya ambaye ni
mkewe ni shabiki wa Jangwani na amekua akimshawishi kila mara kwamba
atue Jangwani ili awe naye karibu zaidi kwani hana mpango wa kuondoka
Dar es Salaam kwenye kazi zake za filamu.
Mchezaji huyo amekiri kushawishiwa mara nyingi
lakini alisema hawezi kujipeleka Yanga mpaka timu hiyo itakapomfuata,
kama hiyo haitoshi aliongeza kwamba anaogopa kuishi Dar es Salaam
kutokana na mambo ya ushirikina yaliyomtokea alipoanza maisha na mkewe
ambaye ameshangaa watu wanaozusha kwamba wameachana.
“Ananitaka nije kucheza Tanzania alikuwa
ananiambia nije Yanga, unajua anaipenda sana Yanga lakini nikamwambia
mimi ni mchezaji ninayejiamini siwezi kuja kuomba Yanga wanisajili acha
waje wao tuzungumze, yuko tayari kufanya hata ushawishi kwa wadau,”
anasisitiza Ndikumana ambaye awali alikuwa akiichezea APOP Kinyras
Peyias ya Cyprus.
Ndikumana alisema kilichomtoa Cyprus na kuja Burundi pamoja na uhusiano wake na Uwoya.
“Kweli nilikuwa Cyprus kama unavyosema lakini
kikubwa ambacho kilinirudisha Tanzania ni pale mke wangu alipokaribia
kujifungua, niliporudi tu baada ya muda nikaanza kuumwa sana na hivyo
kushindwa kurudi Cyprus,” anasimulia.
“Tatizo hilo naweza kusema ni mambo yetu ya
Kiswahili na ni huko Tanzania ndiyo kulikuwa chanzo, kuna vitu vilikuwa
vinanitokea mwilini kiasi kwamba nilikuwa najikuna sana mwili mzima,
hospitali nilikwenda na kupima vipimo vyote hakukuonekana kitu, kuna
wakati wakaniambia ni fangasi.
“Nikaona hapana bora nigeukie upande wa pili wa
tiba asilia, nako hali haikuwa rahisi nilizidi kuteseka ilifikia hatua
najikuna mpaka vidonda vinatoka miguuni nikaona sasa na vidonda hivi
nitarudije Cyprus bora nitibiwe kwanza kabla ya kuondoka.
“Ukweli ni kwamba nilizunguka sana kwa wataalamu
mbalimbali kiu yangu ilikuwa ni kuhakikisha nakuwa sawa, nakumbuka
mwanzoni kama ndani ya miezi miwili nilitumia hadi Sh6milioni kusaka
tiba lakini bado ikashindikana, nilikuwa nataka kuhakikisha napona
haraka ili niwahi kurudi kazini.
“Nilizunguka sana nakumbuka baada ya kuona
Tanzania ni vigumu nikaondoka na kuja hapa Rwanda nako nilitibiwa hali
haikuwa sawa, nikaenda DR Congo kidogo nikapata nafuu lakini baadaye
kuna mtalaamu mmoja akanisaidia tena kwa kiasi kidogo maradhi
yakapungua.
“Kuna mtu namjua kwamba alikuwa akifanya haya
yote, hili nililiamini baada ya kumrudia Mungu, ukiacha ya Mungu pia
hata hao wataalamu karibu wote nilipokuwa napita walikuwa wakimtaja
sioni kama walikuwa wanadanganya kwani ni watu tofauti wote wamemtaja
mtu mmoja, namuachia Mungu na nashukuru sasa nimeanza kurudi katika hali
yangu.
“Baada ya misukosuko yote hiyo Baba yangu
(Ndikumana Kitenge) kule nyumbani ana timu yake ndogo ya vijana, nikawa
natumia muda huo kumsaidia majukumu ya kuwafundisha vijana na hapohapo
na mimi nafanya mazoezi, nilipoona hali imeimarika nikaenda Vital’O
kuwaomba nifanye nao kazi wakakubali na nashukuru walinielewa na
kuniamini sasa nipo nao kwa muda.
“Sijasaini mkataba na Vital’O unajua kuna wakati nafanya
mazoezi kuna timu za Ulaya zilikuwa zinataka kunifuata nikaona niende
Vital’O ili nijiweke sawa endapo watakuja wanikute katika hali nzuri
lakini hao jamaa walivutiwa na mimi wakati nacheza kama beki na sasa
hapa natumika kama kiungo mkabaji sijajua kama wakija watanikubali.”
Alikutana wapi na Uwoya?
“Unajua Irene nilimpenda kupitia filamu
nilipomuona nikataka siku moja nikutane naye, nashukuru Mungu kuna siku
wakati nataka kwenda Kigoma katika harusi ya dada yangu nilipitia Dar es
Salaam nikakutana naye pale uwanja wa ndege.
“Sijabadili dini, ni kweli kwamba tulifunga ndoa
ya kanisani lakini sikubadili dini nilitajwa kwa jina la Hamad
Ndikumana, tulikubaliana na mke wangu tufunge ndoa mbili ya Kikristo na
Kiislamu ikatangulia ile hii nyingine tukasema tutaifunga baadaye lakini
muda ukawa mdogo ila tutaifunga hakuna shida.
Ni kweli wameachana na Uwoya?
“Kwanza nashangaa hao wanaodai nimeachana na mke
wangu wanajua nani amempa talaka mwenzake? Sijaachana na Uwoya, yule ni
mke wangu isipokuwa kwa sasa ni kama tumetengana na huko si kuachana
labda watu wanachanganya mambo.
“Kuna mambo tulishindwa kukubaliana, alikuwa
hataki kuja kuishi na mimi kule Cyprus, alikuwa anataka tuishi Tanzania
tu, sasa mimi kazi yangu ni soka siwezi kuacha kazi ili nirudi Tanzania
niishi na familia yangu bila ya kuwa na kazi hilo lilitufanya tutengane
kidogo.
“Achana na mtoto nipo na maelewano mazuri na Uwoya
hadi sasa tunawasiliana ngoja nikuthibitishie (Anainua simu na kumpigia
lakini haipokelewi) nadhani atakuwa katika kazi zake, yupo safarini
Afrika Kusini amekwenda kurekodi filamu na hata Krish ni mwanangu kila
ninapotaka kumuona namuona bila shida.
“Sasa ana miaka mitatu na tumeshamwanzisha shule,
anasoma (ananionyesha video fupi Krish aliyorekodiwa akihesabu namba kwa
Kiingereza) nadhani sasa utaniamini unajua watu hawajui mimi na Irene
ni wapenzi na tunaonana kila tunapopata nafasi.
“Hayo ni maneno ya watu tu, unajua Tanzania maneno
ni mengi sana, kweli kuna wakati yanasemwa mengi sana ninaposikia
nakutana na mwenzangu namuuliza anakataa lakini ukiacha kukataa kwake
hata mimi nimeshindwa kuthibitisha hayo madai kwa hiyo nayaacha maisha
yanaendelea.
“Kila kitu kina muda wake bado naamini siku moja
nitarudi kuwa karibu na familia yangu, kwa sasa acha kwanza kila mmoja
afanye yake ya kikazi, baadaye tutatulia na kuwa pamoja, watu waache
kutugombanisha,”anasisitiza.
Chanzo: Mwanaspoti
Chanzo: Mwanaspoti